Kigorowa (kinachofahamika pia kama Gorwaa au Kifiomi) ni lugha ya Kikushi cha Kusini inayeongelewa kwenye Bonde la Ufa la Tanzania. Nilisoma Kigorowa kuanzia mwaka 2012 na nimemaliza tasnifu yangu ya PhD kuhusu Kigorowa mwaka 2018. Kinachofuata chini ni utangulizi wa lugha hii.
Aakó Bu’ú Saqwaré anaongea kuhusu kilimo cha katani alipokuwa kijana. [kutoka rekodi ya sauti 20151202g (Harvey 2017)]
Nchi ya kiasili ya Wagorowa ni eneo la Babati mjini pamoja na eneo linalozungusha ziwa Babati. Vijiji vya Wagorowa vinaenda magharibi kutoka hapa mpaka mto Duuru (mto Bubu), na mashariki mpaka mbuga ya wanyama Tarangire. Hakuna mipaka ya kijiografia zingine, na wazungumzaji wa Kigorowa huishi pamoja na wazungumzaji wa Kimbugwe kwenye vijiji kama Magugu kwenye sehemu za kaskazini, na pamoja na wazungumzaji wa Kirangi na Chasi (Alagwa) kwenye sehemu za kusini kama vile Bereko.
Ramani ya nchi ya Gorowa ya kiasili. Ziwa Babati ni katikati, na mto Duuru ni mstari wa kijani kwenye mashariki. Picha kutoka Google Maps
Bado watafiti hawajahesabu idadi ya watu wanaozungumza Kigorowa, lakini kupatana na data za sensa pamoja na uangalizi, nakadiri kwamba idadi ya wazungumzaji wa Kigorowa haiwezi kupita watu 133,000.
Kutoka jumla hii, nakadiri tena kwamba idadi ya wazungumzaji wa Kigorowa wanaokitumia mara kwa mara ni takriban 80,000. Yaani, hata kama watu wanajua Kigorowa, kwa sababu mbalimbali, hawakitumii. Kwa mfano, mzungumzaji fulani wa Kigorowa anaweza kuacha Kigorowa akiishi pamoja na watu ambao hawaongei Kigorowa; anaweza kuacha Kigorowa akifanya kazi ambaye Kigorowa hakihusiki (kwa mfano, kwenye ofisi ya serikali, au kanisani); anaweza kuacha Kigorowa akiona lugha hii kama ni mbaya au sio kamili. Inaonekana kwamba ni muungano wa sababu haya, pamoja na zingine, zinazopunguza tamaa kutumia Kigorowa, na sasa ni kawaida sana kuona wazungumzaji wa Kigorowa kutumia Kiswahili kuwasiliana kwenye maisha ya kila siku. Kigorowa hakifundishwi shuleni, na kwa kawaida hakiandikwi. Idadi ya watu wanaojifunza lugha ya Kigorowa inaendelea kupungua (hasa kwenye sehemu za mjini kama Babati mjini) na kwa sababu hizi, Kigorowa kinaweza kuitwa lugha kwenye hatari ya kupotezwa.
Picha ya Aamaa Mando’o Silo kwenye bohari lake la nafaka, tarehe 6, mwezi wa 10, mwaka 2016. [Picha 20161006g (Harvey 2017)]
Kama makabila mengine kwenye eneo hili, Wagorowa wanajua kwamba hawajakaa kwenye nchi yao kwa milele, na hukumbuka wakati walipoishi sehemu tofauti. Wakati ule, hadithi zinasema kwamba Wagorowa, Wairaqw, Waasi (Alagwa) na Waburunge waliishi pamoja kama ndugu. Hisia hii ya asili moja haishangazi: makabila haya wote yanatumia lugha zinazofanana (Kikushi cha Kusini), na utamaduni zao zinafanana kwenye namna muhimu.
Kwa kiasi kubwa, Wagorowa wa leo ni wakulima wanaofuga mifugo pia (hasa kondoo, mbuzi, na ng’ombe wa kiasili). Kati ya mazao muhimu ni mtama na maboga. Lakini, ufugaji unashika sehemu muhimu sana kwenye utamaduni wa Kigorowa, na Wagorowa wengi wanajitambulisha kwanza kama wafugaji, kabla ya kama wakulima. Wagorowa wengi ni Wakristo, pamoja na idadi kubwa ya Waislamu. Hizi dini zipya zimekopa sehemu muhimu kutoka imani ya kiasili, na dini zipya pamoja na imani ya kiasili huendelea pamoja.
Picha ya ziwa Babati iliyechukuliwa kutoka kusini, kwenye njia ya Endagwe. Mwaka 2012.
Kigorowa ni lugha ya Kikushi (kama vile Kioromo na Kisomali), kwenye tawi la Kikushi cha Kusini (pamoja na Kiiraqw, Chasi (Alagwa) na Kiburunge). Kifonetiki, Kigorowa ni lugha yenye sauti za koromeo (pharyngeal sounds), na konsonanti pacha (geminate consonants). Ina irabu fupi na ndefu, pamoja na mfumo kidatu lafudhi (pitch-accent system) yenye kidatu kinachopanda na kidatu cha kawaida (rising pitch accent, level pitch accent). Hii tofauti kati irabu inatumika sana kwenye upatanifu wa vitenzi. Kimofolojia, nomino za Kigorowa zina mambo mengi: huweza kuwa na thamani ya umoja, wingi, au kutokuwa na thamani ya namba yeyote (na kama ziko hivo zinamaanisha kundi la kitu). Jinsia la kisarufi (la kiume, la kike, au la kati) linategemea kiambishi tamati ya namba kwenye nomino: kwa hiyo, jinsia la nomino inaweza kubadilisha kufuata thamani ya kiambishi tamati. Desi ‘msichana’ kwenye Kigorowa ina jinsia la kisarufi la kike, lakini desu ‘wasichana’ ina jinsia la kisarufi la kiume. Kisintaksi, vishazi (clauses) vyote vya Kigorowa (kasoro agizi) vina kisaidizi (auxiliary) kinachobeba taarifa nyingi ya kisarufi. Upande wa usemi (discourse), taratibu ya maneno (word order) kwenye Kigorowa ni huru zaidi kuliko Kiiraqw, na inatumia taratibu tofauti kutenda kazi za amali (pragmatic effects). Mitindo ya lugha ya kutazamisha kwenye Kigorowa ni kama vile mafumbo, uaguzi kwa kuzungumza na mawe, na taratibu kubwa sana ya nyimbo.